Umuhimu wa utafiti wa kifonetiki
Kati ya matawi hayo matatu, Fonetiki-tamshi ndilo tawi ambalo
limechunguzwa kwa undani zaidi na kwa muda mrefu sana (hasa kutokana na
changamoto iliyotokana na kugundulika kwa sarufi ya Sanskrit na wanazuoni wa
nchi za Ulaya Magharibi katika kame ya kumi na nane, kama tulivyosema hapo
mwanzo). Istilahi nyingi za kifonetiki zinazotumiwa na wanaisimu zinahusiana na
tawi hili. Katika sura hii, hili ndilo tawi ambalo tutaliangalia.
Hata hivyo, uchunguzi uliofanywa katika Fonetiki-safirishi
umesaidia sana katika kutia nguvu baadhi ya mahitimisho yaliyofikiwa na
wataalamu wa Fonetiki-tamshi. Kwa mfano:-
i) imethibitika kuwa kila sauti inayotolewa na kiungo-sauti cha mwanadamu ni tofauti na nyingine kwa kiasi fulani. Hivyo sifa bainifu zinazotolewa kuhusu foni (kama tutakavyoona hivi punde) ni za wastani, na kuna mambo mengi ambayo yanaachwa, mambo ambayo mwanafonetiki anaona kuwa hayasaidii katika kufanikisha mawasiliano kati ya wajua-lugba. Ni wazi, kwa mfano, kuwa kuna tofauti kati ya matamshi ya mtu mwenye furaha, mwenye huzuni, mwenye mafua, au mgojwa taabani. Lakini wote bawa, ikiwa lugha wanayozungumza ni Kiswahili, wakitamka neno ‘mwanangu’ litasikika kuwa ni neno hilo hilo, yaani wote watalipa maana moja. Tofauti za matamshi zinazotokana na hali za wazungumzaji haziingizwi katika uchambuzi wa fonetiki-tamshi. Vivyo hivyo, neno rahisi la Kiswahili kama ‘kiti’ linaweza kutamkwa kwa njia tofauti na wazungumzaji tofauti au na mzungumzaji huyo huyo katika wakati na mazingira tofauti: [khiti], [kithi], au [kiti]. Matamshi ya kwanza ya neno hilo yana mpumuo katika kipasuo [k], matamshi ya pili yanaweka mpumuo katika kipasuo [t], na matamshi ya tatu hayana mpumuo popote. Katika Kiswahili Sanifu mpumuo si sifa inayotofautisha maneno, yaani si sifa bainifu. Lakini sifa hiyo hiyo ya mpumuo ni muhimu katika lugha nyingine kama vile Kihindi na Kiswahili cha Pemba (Kipemba). Kwa sababu hiyo, wanafonetiki ni lazima waonyeshe tofauti hiyo kati ya sauti.
ii) Fonetiki-safirishi imethibitisha dai la fonetiki-tamshi kuwa semi zinapotamkwa, hazikatwikatwi katika sauti moja moja kama mazoea yetu ya maandishi (na hata ya alama za IPA) yanavyotushawishi Kama vile mawimbi yanavyosafirishwa hewani, semi pia huundwa na mfululizo wa sauti. Hivyo mikato tunayoiweka kati ya sauti moja na nyingine ni ya kukadiria kwa kiasi, kikubwa. Kwa mfano, katika neno baba si rahisi kujua hasa [b] inaishia wapi na [a] inaanzia wapi. Ndiyo sababu inakuwa vigumu kutamka sauti konsonanti nyingine bila kuziwekea irabu (bila shaka unakumbuka jinsi ulivyofundishwa alfabeti shuleni!). Ni kweli pia kwamba sauti zinazofuatana katika matamsbi huathiriana sana. Hali hii huongeza ugumu wa kuziainisha.
Katika Fonetiki-tamshi, sauti zinaainishwa kufuatana na vigezo
vikuu viwili:
a) Mahali zinapotamkiwa - yaani ni viungo-sauti vipi vinatumika katika utoaji wa sauti hizo.
b) Jinsi zinavyotamkwa - yaani kunatokea nini wakati hewa inatoka mapafuni kupitia kwenye ‘mrija-hewa’, kupitia kwenye glota, mpaka kufikia kwenye ‘mkondo-sauti’. Katika sehemu zifuatazo, vigezo hivi vitachunguzwa kwa undani.
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni